April 26 mwaka 1991, Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi nchini Kenya umefurika watu kiasi ambacho inadaiwa haikuwahi kutokea.. Kisa ? Mwanamuziki nyota nchini Congo DRC, Kanda Bongoman anajiandaa kufanya tamasha la muziki. Wakati tamasha likiwa limepamba moto, ghafla taarifa ya serikali kupitia vyombo vya habari inatoka kuwa Rais wa Kenya, Daniel Arap Moi amempa mwanamuziki huyo saa 24 kuondoka nchini humo na kumuita "Tapeli mkubwa". Hasira za Moi kumtimua Bongoman ndani ya saa 24 zilitokana na Rais huyo kushindwa kuwapata viongozi waandamizi wa chama cha KANU na serikali katika kikao alichokiitisha ghafla kwa sababu ya uwepo wa jambo la dharura. Kwa bahati mbaya, viongozi waandamizi wote walioitwa kikaoni na Rais Moi walishindwa kupatatikana sababu ya kuudhuria tamasha la mwanamuziki Kanda Bongoman na hivyo kujikuta akibaki peke yake na watumishi wachache kikaoni. Lakini, nyuma ya amri ya Rais Moi kumfurusha Bongoman inadaiwa kuwepo kwa 'Chuki binafsi' za mtu wake wa karibu, aliyekuwa Mkuu wa Usalama wa Ikulu, Bw Hezekiah Ogengo Oyugi. Inaelezwa Bw Oyugi ndiye 'aliyeinjinia' amri ya Bongoman kutimuliwa baada ya mwanamuziki huyo kugoma kutumbuiza kwenye birthday ya binti wa kiongozi huyo, kutokana na kuwa na ratiba ngumu ya kutumbuiza kwenye matamasha yake. Kufukuzwa kwa Bongoman pia hakukuwaacha salama maafisa waandamizi wa chama cha KANU na Serikali, ambao na wao wakaingizwa kwenye mgogoro mkubwa na baadhi kufurushwa kutokana na 'kugomea' wito wa kuhudhuria kikao cha Rais. Lakini marufuku hiyo kwa Bongoman ni kama ilichangia kumpa "Promo". Habari zilivuma Afrika nzima, na kila shabiki akataka kujionea, ni nini haswa hicho kilichopelekea mpaka viongozi wa Kenya kugomea wito wa Rais sababu ya mwanamuziki huyo.? Tanzania ikawemo kwenye foleni ya kuchangamkia fursa ya kuhitaji huduma ya Kanda Bongoman. Bongo Man akatua nchini na Tamasha likaandaliwa kwenye hoteli ya Kilimanjaro jijini Dar ambapo huko ndipo historia nyingine ilipoanza kuandikwa. Tiketi za kumuona mwanamuziki huyo zilikuwa 100 tu, na kila tiketi moja iliuzwa kwa Shilingi Laki Moja (100,000) za kitanzania. Katika hali ya kushangaza, tiketi hizo ziliisha mapema mno na watu kurudi na pesa zao mkononi. Ikumbukwe kiingilio shilingi LAKI MOJA kwa mwaka 1992.. Imagine that.! Malalamiko ya baadhi ya mashabiki kushindwa kumuona Bongoman Kilimanjaro Hoteli yakazidi, hali hiyo ikalazimu kuandaliwa onesho lingine kwenye Uwanja wa Taifa (Uhuru) ili kutoa fursa kwa watu wengi zaidi kumuona mwanamuziki huyo. Wakati haya yakiendelea, Taifa lilikuwa kwenye mgogoro mkubwa wa mgomo wa madaktari ulikuwa umetangazwa nchi nzima kutokana na madaktari kushinikiza madai ya ongezeko la mishahara yao waliyokuwa wakiipigania kupanda kwa muda mrefu. Nchi ikawa kwenye sintofahamu hiyo kubwa, Rais Ali Hassan Mwinyi akaitisha mazungumzo na madaktari hao kwa ajili ya kutafuta suluhisho la mgomo wao ulioonekana kuiathiri nchi kwa sehemu kubwa katika kipindi kifupi sana. Pamoja na Taifa kuwepo kwenye taharuki kutokana na mgomo huo, uwepo wa Bongoman ulionekana kama kuwa juu ya kila kitu. Rais Mwinyi akiwa anasubiriwa na madaktari waliogoma kikaoni, akapitia kwanza kuhudhuria shoo ya Bongoman pale 'Shamba la Bibi'. Baada ya kukaa pale kwa muda kadhaa, ndipo msafara wake ukatoka kuelekea kukutana na madaktari waliogoma kwa ajili ya mazungumzo ya kutafuta suluhu. Jambo hilo likalaumiwa na wengi, kwanini Bongoman apewe kipaumbele kuliko Watanzania wanaoathirika na mgomo wa madaktari. Watanzania wakaanza kufanana akili zao na Rais Moi. Wengi wakasema (kumbe) Moi alikuwa sahihi kumfurusha mwanamuziki huyo, kwa sababu uwepo wake kwenye nchini unaweza kuwafanya viongozi kushindwa kuona mambo mengine muhimu yanalolikabili Taifa. Lakini pamoja na yote, umahiri wa mwanamuziki huyo ndiyo uliopelekea yote hayo kutokea, kwani kipaji chake cha hali ya juu kilikuwa juu ya vichwa vya watu wengi wenye maarifa, nyakati zake zilikuwa bora na sahihi zaidi kwa wakati huo pengine kuliko wakati wowote mwingine kwake. Bongoman alionewa tu.! Kwa nyimbo zile za "Sai" "Monie" "Isambe" "Bili" "Muchana" "Yesu Kristo" "Sana" "Wallowi" na nyinginezo, unaanzaje kuondoka jukwaani ukamsikilize Mzee Nyayo akikupa maagizo anayoweza kukupa hata baadae ukishamaliza kupata burudani ? Rais Mwinyi naye ni binadamu pia. Kiingilio cha shilingi Laki Moja mwaka 1992 na tiketi zote 100 kwisha huku watu wakirudi na hela zao mkononi, unadhani haikumshtua kuhitaji kumwona live huyo Bongoman anaonekaje ? Kama ungekuwepo wakati ule, comment yako ingeweza kuwa tofauti na hii utakayoiandika sasa. Naumia mno napoona nyakati za wanamuziki mahiri wa Congo zimefunikwa na kizazi cha wanamuziki wao wa sasa, wanaoshindana kufuga na kurembesha Ndevu. Nyakati.!
0 Comments