Akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa ahadi ya kuhakikisha vijana wanapata nafasi kamili ya kushiriki katika kujenga mustakabali wa taifa kupitia ushirikishwaji wa moja kwa moja katika masuala yao ya maendeleo.
Rais Samia alisema kuwa licha ya kuwepo kwa majukwaa mbalimbali ya kuhimiza ushiriki wa vijana, mara nyingi shughuli hizo zimefifishwa na kuingiliwa na masuala ya kisiasa, hali inayopunguza mvuto na malengo ya majukwaa hayo.
“Ili
kuhakikisha vijana wanapata nafasi kushiriki katika kujenga mustakabali
mwema wa taifa letu, tutaweka kipaumbele kwenye ushirikishwaji wa
vijana katika masuala ya maendeleo yao. Mimi na wenzangu serikalini
tumefikiria kuwa na Wizara kamili itakayoshughulikia mambo ya vijana, na
vilevile ninafikiria kuwa na washauri wa masuala ya vijana ndani ya
Ofisi ya Rais.”
Rais Samia alibainisha kuwa hatua hiyo inalenga
kutoa mwongozo wa moja kwa moja kwa vijana, kuongeza ushiriki wao katika
maamuzi ya kitaifa, na kuhakikisha sauti yao inahusishwa kikamilifu
katika sera na mipango ya maendeleo ya taifa.
Aidha, amesema
kuwa hatua hiyo itasaidia kukuza vipaji vya vijana na kuimarisha mchango
wao katika maendeleo endelevu ya Tanzania.
Tags
Habari
