Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Novemba 11, 2025 limefanya ziara maalum nyumbani kwa Makamu wa Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, eneo la Mayamaya mkoani Dodoma, ambapo mazungumzo yenye tija kubwa kuhusu hali ya mazingira nchini yamefanyika.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Mpango ameelezea kwa kina wasiwasi wake kuhusu kasi ya uharibifu wa mazingira unaoendelea kushamiri nchini, huku akisisitiza haja ya kuwepo kwa msukumo mkubwa zaidi katika kulinda maeneo ya hifadhi na kusimamia matumizi bora ya ardhi.
Amesema kuwa maeneo mengi ya hifadhi yamekuwa yakivamiwa, mito mingi imechepushwa kinyume na taratibu, huku mabwawa ya kuzalisha umeme yakikumbwa na uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu. Vilevile, biashara ya mbao na mkaa imeendelea kuchangia ongezeko la ukataji miti na hivyo kuongeza kasi ya uharibifu wa misitu nchini.
Dkt. Mpango amebainisha kuwa changamoto za mifugo isiyo na utaratibu mzuri, uchimbaji holela wa mashamba, pamoja na tatizo la mimea vamizi, vinahitaji mikakati madhubuti ya kitaifa. Amesisitiza kuwa NEMC inapaswa kupewa nguvu zaidi katika utekelezaji wa Sheria na Kanuni za mazingira, akisema: “Sauti ya NEMC isiwe tena sauti ya mtu aliye nyikani.”
Aidha, Dkt. Mpango ametoa wito kwa Serikali na jamii kwa ujumla kutekeleza kwa vitendo mpango wa Kijanisha mazingira “Greening the Environment”, huku akipendekeza kuanzishwa kwa green parks na botanical gardens katika Majiji na Miji mikuu ya nchi, kama sehemu ya kujenga miji yenye mazingira rafiki na yenye afya.
“Ni lazima tujiulize kama Taifa, kama miji, tumechukua hatua gani za kulinda na kurejesha uoto wa asili? Inawezekana kabisa kuwa na mazingira mazuri kama tukidhibiti shughuli zetu kwa kufuata sheria na mipango tuliyojiwekea,” amesisitiza Dkt. Mpango.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi alipozungumza alipongeza maono na ushauri uliotolewa Dkt. Mpango, huku akiahidi kuendelea kutumia maarifa hayo katika kuimarisha juhudi za Hifadhi na Usimamizi endelevu wa mazingira nchini.
Ziara hiyo iliyofanywa na Menejimenti ya Baraza imekuwa ni ya muhimu katika kujenga mashirikiano kati ya Taasisi za Serikali na viongozi wastaafu wenye uzoefu mkubwa, kwa lengo la kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa nchi yenye mazingira safi, salama, na yenye uendelevu wa kiikolojia.






