Aliyekuwa
waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga amelaani vikali wito wa waziri wa
usalama nchini Kenya Kipchumba Murkomen kwa polisi kuwafyatulia risasi
watu watakaojaribu kukaribia vituo vya polisi na kuongeza kuwa
anayewataka polisi kufyatulia raia risasi anapaswa kulaaniwa vikali.
Hatua
hii inatajwa kuwa kama ukosoaji wa nadra kwa utawala wa Rais William
Ruto hasa kwasababu chama cha Bwana Odinga kina wanachama wake watano
wanaohudumu katika baraza la mawaziri katika mpango wa serikali ya
muungano a maarufu ''broad based government.''
Waziri Murkomen
alisema alitoa agizo hilo baada ya vituo vya polisi kushambuliwa wakati
wa maandamano siku ya Jumatano, lakini matamshi yake yalitafsiriwa
vibaya.
Murkomen alisema kauli zake ziliambatana na Kifungu B(1)
cha Sheria ya Huduma ya Polisi ya Kitaifa, ambayo inaruhusu maafisa
kutumia bunduki kujilinda au kuwalinda wengine dhidi ya vitisho vya kifo
au majeraha mabaya.
Odinga pia alizungumzia matukio ya
maandamano ya Juni 25, ambapo watu kadhaa walipoteza maisha huku
akilaani wahalifu walioingilia maandamano hayo na kupora na kuharibu
mali ya umma.
Aidha alitoa wito wa kuwepo kwa mazungumzo ya
kitaifa, akiwataka wananchi na viongozi kufanya mazungumzo yenye maana
ili kuandaa njia ya umoja nchini.