JAJI MKUU: HATUTARUHUSU WATU KUITISHA MAHAKAMA

 

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju, amesema vitendo vya kuidharau na kuitisha Mahakama havitavumiliwa wala kupewa nafasi, akisisitiza umuhimu wa kulinda amani na utawala wa sheria nchini.

Jaji Masaju ameyasema hayo Agosti 31, 2026, wakati akifungua semina elekezi kwa Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu, ambapo aliwataka watendaji hao kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya Katiba na viapo vyao.
 
Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Mkuu alionya kuwa Mahakama haitaruhusu vitendo ambavyo vinaweza kuhatarisha utulivu na kufanya taifa kushindwa kutawalika, akisisitiza kuwa amani ni msingi muhimu wa taifa.
 
“Hatutaruhusu watu kuidharau Mahakama, kuitisha hii Mahakama nchi itatawalikaje? Tunahitaji amani. Kwa hiyo mtakuwa macho kwenye hili. Hatutaendekeza kitendo ambacho kitafanya taifa hili lisitawalike kwa kile kinachoitwa kutetea haki za binadamu,” amesema Masaju.
 
Aidha, Jaji Mkuu amewataka Naibu Wasajili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia Katiba pamoja na viapo vyao, huku wakilinda heshima na mamlaka ya Mahakama.
 
Kauli hiyo imekuja wakati ambapo suala la heshima kwa Mahakama, utawala wa sheria na ulinzi wa amani likisisitizwa katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi za haki nchini.

Post a Comment

0 Comments