Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei mpya za bidhaa za mafuta ya petroli nchini, zitakazoanza kutumika kuanzia Jumatano, Septemba 2, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa ya EWURA, bei za mafuta nchini kwa mwezi Septemba zimeshuka kwa Shilingi 102 kwa lita moja ya petroli na Shilingi 101 kwa lita ya dizeli, hatua inayotajwa kuchangiwa na juhudi mbalimbali za Serikali za kuhakikisha bei za mafuta zinakuwa himilivu.
Katika jiji la Dar es Salaam, bei ya juu ya rejareja kwa lita moja ya petroli imewekwa kuwa Sh3,796, huku dizeli ikiuzwa kwa Sh3,877 na mafuta ya taa kwa Sh3,713.Kwa upande wa Tanga, lita moja ya petroli itauzwa kwa bei isiyozidi Sh3,872, dizeli Sh3,953 na mafuta ya taa Sh3,789.Mkoani Mtwara, bei ya petroli imewekwa kuwa Sh3,909 kwa lita, dizeli Sh3,990 na mafuta ya taa Sh3,825.
EWURA imewataka wafanyabiashara wa mafuta kuzingatia viwango hivyo na kuhakikisha bidhaa zinauzwa kwa bei zisizozidi bei elekezi zilizotangazwa.Mamlaka hiyo imeonya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mfanyabiashara yeyote atakayekiuka agizo hilo.
EWURA pia inaeleza kuwa bei kikomo za mafuta hutangazwa kila mwezi na zinatumika kama kiwango cha juu ambacho vituo vya mafuta haviruhusiwi kukivuka katika maeneo yao.

0 Comments