Serikali imesema imeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu kwa kufanikiwa kuwaokoa jumla ya wahanga 160. Kati yao, wahanga 126 waliokolewa wakiwa ndani ya Tanzania kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi, huku wengine 34 wakirejeshwa nchini baada ya kuokolewa kutoka mataifa mbalimbali walikokuwa wamepelekwa.
Taarifa hiyo imetolewa wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupinga Usafirishaji Haramu wa Binadamu, ambayo mwaka huu imebeba kaulimbiu isemayo, "Jihadhari na Utumwa Kupitia Utapeli Mitandaoni." Kaulimbiu hiyo inalenga kuhamasisha jamii kutambua mbinu mpya zinazotumiwa na wahalifu kuwavuta watu kwenye vitendo vya usafirishaji haramu kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali.
Akizungumza wakati wa kutoa tamko la maadhimisho hayo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesema juhudi za vyombo vya dola zimewezesha kukamatwa kwa jumla ya watuhumiwa 57 wanaodaiwa kuhusika na biashara hiyo haramu.
Kwa mujibu wa Waziri Katambi, kati ya watuhumiwa hao, 45 tayari wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili, huku watuhumiwa wengine 12 wakiendelea kufanyiwa uchunguzi na upelelezi kabla ya hatua zaidi za kisheria kuchukuliwa.
Serikali imewahimiza wananchi kuwa makini na ahadi za ajira, masomo au fursa nyingine zinazotolewa kupitia mitandao bila uhakiki, ikisisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi na vyombo vya usalama ni muhimu katika kutokomeza tatizo la usafirishaji haramu wa binadamu nchini.

0 Comments