Mjumbe wa Kudumu wa Kamati Kuu na Mwenyekiti Mstaafu wa CHADEMA, Freeman Mbowe, amepongeza kukamilika kwa Mradi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP), akisema ni mradi mkubwa wa kihistoria na fahari kwa Tanzania.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo, Mbowe amesema JNHPP ni miongoni mwa miradi mikubwa iliyowahi kutekelezwa nchini tangu Uhuru, huku akitoa pongezi kwa viongozi waliotangulia pamoja na Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza mradi huo hadi kukamilika.
Mbowe amesema matarajio ya Watanzania ni kuona umeme unaozalishwa na JNHPP ukitumika zaidi ya kuwasha taa, bali kuwa kichocheo cha maendeleo ya viwanda, huduma za kijamii, uzalishaji na ukuaji wa uchumi.
Amesema upatikanaji wa umeme wa uhakika unapaswa kuongeza uzalishaji na kuchochea uwekezaji, ajira na shughuli mbalimbali za kiuchumi nchini.
Aidha, Mbowe amesisitiza kuwa mafanikio ya kukamilika kwa mradi huo ni ya taifa zima, huku akiwapongeza Watanzania pamoja na watendaji wa TANESCO kwa mchango wao katika kufanikisha mradi huo.

0 Comments