MATOKEO YA NBC: SIMBA NA MBEYA CITY ZASHINDA, SINGIDA YASARE

Na Ally Mandai. 

Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara imeendelea leo Jumatano kwa michezo mitatu kuchezwa katika viwanja tofauti nchini, huku Simba SC ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Pamba Jiji.

Mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, uliishuhudia Simba SC ikipata pointi tatu muhimu baada ya kuifunga Pamba Jiji mabao 2-1 katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa.

Katika mchezo mwingine uliopigwa mapema kwenye Uwanja wa CCM Sokoine jijini Mbeya, wenyeji Mbeya City wamerejesha ari na nguvu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji.

Ushindi huo umeifanya Mbeya City kuondoka na pointi zote tatu mbele ya mashabiki wake, huku Dodoma Jiji ikikosa nafasi ya kupata pointi katika mchezo huo wa ligi.

Mchezo wa mwisho wa siku umefanyika katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, ambapo Kagera Sugar na Singida wamegawana pointi baada ya kutoka sare ya bao 1-1.

Matokeo hayo yanaendelea kuongeza ushindani katika Ligi Kuu Tanzania Bara, huku kila timu ikisaka pointi muhimu katika mbio za kujiimarisha kwenye msimamo wa ligi.

Post a Comment

0 Comments