MAJI UHAKIKA DAR NA PWANI PAMPU MPYA ZAFUNGWA

Uwekezaji wa shilingi bilioni 16 uliofanywa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) katika ununuzi wa pampu mpya nane unatarajiwa kuongeza uwezo wa uzalishaji na usafirishaji wa maji, hatua inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa Dar es Salaam na Pwani.

Hayo yabainishwa, wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mazingira na Maji, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Jackson Kiswaga, ilipotembelea na kukagua Mtambo wa Uzalishaji Maji Ruvu Juu uliopo Mlandizi, Mkoa wa Pwani, kujionea hali ya uzalishaji, uendeshaji pamoja na maendeleo ya ufungaji wa pampu hizo.

Kwa mwananchi, uwekezaji huo unalenga kuongeza uwezo wa maji yanayochukuliwa na kusafirishwa kutoka chanzo hadi mtamboni, hivyo kuwezesha DAWASA kuzalisha na kusambaza maji kwa ufanisi zaidi.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mhe. Kiswaga amesema Kamati imeridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha miundombinu ya maji, hususan uwekezaji katika pampu mpya unaolenga kuongeza ufanisi wa huduma. 

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, amesema Mamlaka imenunua pampu mpya nane kwa gharama ya shilingi bilioni 16. Kati ya hizo, pampu sita tayari zimewasili, huku mbili zikiwa katika mchakato wa kuwasili.

Amesema pampu saba kati ya hizo zimepangwa kufungwa katika Mtambo wa Ruvu Juu, ambapo nne zitafungwa katika eneo la uchukuaji na usafirishaji wa maji ghafi, huku tatu zikiwa zimepangwa kufungwa katika eneo la mtambo.


Kwa sasa, pampu mbili tayari zimefungwa katika eneo la uchukuaji na usafirishaji wa maji ghafi, huku nyingine mbili zikiwa zimefungwa katika eneo la mtambo. Kazi ya kufunga pampu zilizosalia inaendelea.

Post a Comment

0 Comments