Kwa mara ya
kwanza, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imefanikiwa kumfanyia
upasuaji wa moyo bila kufungua kifua mtoto mwenye umri wa siku mbili tu
aliyezaliwa akiwa na tatizo la kubana kwa mshipa unaopeleka damu kwenye
mapafu.
Upasuaji huo wa kihistoria kwa kutumia mtambo wa Cathlab
umefanyika wakati wa kambi maalum ya siku sita iliyoendeshwa na
wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na mradi wa Little Heart kutoka
Shirika la Muntada Aid la nchini Uingereza.
Akizungumza jijini
Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa JKCI, Dkt. Angela Muhozya, ameeleza
kuwa kambi hiyo imefanikisha upasuaji kwa jumla ya watoto 44, ambapo 28
walifanyiwa upasuaji kwa njia ya tundu dogo na 16 upasuaji mkubwa wa
kufungua kifua, huku shirika hilo likichangia vifaa tiba vya thamani ya
shilingi milioni 50.
Dkt. Angela ametoa rai kwa wajawazito na
wazazi kufanya uchunguzi wa mapema wa magonjwa ya moyo kwa watoto ili
kuokoa maisha yao na kuepuka kufika hospitalini wakati ugonjwa ukiwa
umefikia hatua mbaya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa
Shirika la Muntada Aid, Nayaf Sheikh, amepongeza miundombinu bora na
utaalamu wa JKCI akieleza kuwa ubora wa taasisi hiyo unaondoa ulazima
kwa wananchi wa Tanzania na ukanda mzima wa Afrika Mashariki kusafiri
nje ya nchi kufuata huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.
0 Comments