Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ametoa onyo kwa watu waliohusika na vurugu za Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan haitampendelea mtu yeyote katika mchakato wa kutoa haki.
Akizungumza jana katika Kijiji cha Kangagani, Kaskazini Pemba, wakati akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la Skuli ya Amali inayojengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 4, Waziri Katambi alitoa ufafanuzi kuhusu tume zilizoundwa na Rais kuchunguza vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi wa Oktoba 29.
Waziri Katambi amesema kuundwa kwa tume hizo ni hitaji la sheria za kitaifa na kimataifa, ili Tanzania iweze kuanza kuchukua hatua yenyewe katika kushughulikia masuala yanayohusiana na vurugu hizo.
Ameeleza kuwa baada ya Tume ya Jaji Chande kukamilisha kazi ya kutafuta ukweli kuhusu yaliyotokea, sasa Tume ya Jaji Lila imeanza kazi ya kushughulikia masuala ya kijinai yanayohusiana na tukio hilo.
Akisisitiza msimamo wa Serikali kuhusu usawa mbele ya sheria, Waziri Katambi amesema, “Ndugu zangu Watanzania niwaambie na niwahakikishie serikali iko very serious na jambo hili. Hatutapendelea mtu, hata kama ni Katambi anahusika atawajibika. Sheria ni msumeno. Yeyote ambaye anahusika... awe kiongozi wa serikali, awe ni kiongozi mtu binafsi, awe yoyote, awe ni raia aliyehusika katika changamoto hizo tulizokwenda kuzipata, atawajibika kwa mujibu wa sheria”



0 Comments