Kamanda
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Jumanne Muliro ametangaza
kuanza kwa operesheni maalumu dhidi ya Makundi ya matapeli
wanaojihusisha na vitendo vya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu,
akisema Jeshi la Polisi limetangaza “kiama cha kisheria” dhidi yao.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari leo Agosti 4, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa
Central Police Jijini Dar es salaam, SACP Muliro amesema matapeli hao
hutumia mbinu mbalimbali kuwalaghai Wananchi, ikiwemo kujifanya
Wafanyabiashara wa madini, Wauzaji wa magari na viwanja, Wanunuzi wa
mazao kama korosho na dengu, pamoja na watoa huduma za usafirishaji wa
mizigo, kisha kutoweka baada ya kupokea fedha kutoka kwa waathirika.
Amesema
Jeshi la Polisi limeendelea kupokea malalamiko kutoka maeneo mbalimbali
Nchini, yakiwemo Newala, Kibondo, Kasulu na Mbinga kuhusu Wananchi
waliopoteza fedha kupitia udanganyifu huo.
Kutokana na hali hiyo,
Muliro amesema operesheni hiyo itaendelea hadi Watuhumiwa wote
watakapobainika na kufikishwa kwenye Vyombo vya Sheria, akisisitiza kuwa
Jeshi la Polisi halitavumilia vitendo vinavyowaumiza wananchi na
kuhatarisha usalama wa uchumi.
Aidha, ametoa wito kwa Wananchi
kuendelea kutoa taarifa kuhusu viashiria vya uhalifu ili kusaidia kuzuia
na kudhibiti matukio ya kihalifu kabla hayajatokea.
0 Comments