Na Ally Mandai.
Klabu ya Simba SC leo imeanza rasmi zoezi la kutambulisha wachezaji wapya waliowasili kujiunga na kikosi hicho kwa ajili ya msimu wa 2026/2027, huku kiungo mkabaji wa Kitanzania Kelvin Nashon akiwa mchezaji wa kwanza kutambulishwa rasmi.
GUSA HAPA,REJESHA KUJIAMINI CHUMBANI NA VIKSI LOTION
Kelvin Nashon ametua Simba akitokea Pamba Jiji FC, ambapo alionyesha kiwango kizuri msimu uliopita na kujijengea sifa kama mmoja wa viungo bora wa ukabaji nchini. Uwezo wake wa kukaba, kuvunja mashambulizi ya wapinzani, pamoja na kuanzisha mashambulizi kutoka eneo la kiungo ulimfanya kuwa miongoni mwa wachezaji waliovutia macho ya vigogo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Usajili wa Nashon unaonekana kuwa sehemu ya mkakati wa Simba kuimarisha safu ya kiungo kuelekea mashindano ya ndani na kimataifa msimu ujao. Kiungo huyo pia aliwahi kuitwa katika kikosi cha Taifa Stars kutokana na kiwango chake bora akiwa na Pamba Jiji, jambo lililoonyesha maendeleo yake katika soka la Tanzania.
Mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi sasa wanasubiri kuona ni wachezaji gani wengine watakaotambulishwa katika siku zijazo, huku klabu hiyo ikiendelea na maboresho ya kikosi chake kwa lengo la kurejesha ubingwa wa Ligi Kuu na kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa msimu wa 2026/2027.

0 Comments