Na Ally Mandai
Macho na masikio ya mashabiki wa soka nchini sasa yanaelekezwa kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la CRDB Federation Cup msimu huu utakaowakutanisha vigogo wawili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC na Azam FC.
Simba SC imefanikiwa kutinga hatua ya fainali baada ya kuonyesha ubora mkubwa katika mchezo wa nusu fainali kwa kuichapa Coastal Union mabao 4-0 katika mechi iliyopigwa kwa ushindani mkubwa. Ushindi huo uliwapa Wekundu wa Msimbazi tiketi ya moja kwa moja ya kucheza fainali huku wakionyesha dhamira ya kutwaa taji hilo.
Kwa upande wa Azam FC, wao wamepata nafasi ya kucheza fainali baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Yanga SC, katika mchezo wa kusisimua wa nusu fainali ulioshuhudia timu zote zikionesha kiwango cha hali ya juu.
Fainali hiyo inatarajiwa kuwa ya ushindani mkubwa kutokana na ubora wa vikosi vya timu zote mbili pamoja na historia ya mikutano yao katika mashindano mbalimbali. Simba SC itakuwa ikisaka kuongeza taji jingine katika kabati lake la mataji, huku Azam FC ikilenga kuandika historia mpya kwa kutwaa ubingwa huo mbele ya Simba Sc.
Mashabiki wa soka nchini wanatarajia kushuhudia pambano kali litakaloamua bingwa mpya wa CRDB Federation Cup msimu wa 2025/2026, huku timu zote zikiahidi kutoa burudani ya hali ya juu katika dakika 90 za mchezo huo muhimu.

0 Comments