SERIKALI IMETOA BILIONI 196 KUIMARISHA MIUNDOMBINU YA ELIMU MWANZA- RC MTANDA

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema katika kuimarisha sekta ya elimu Mkoani humo, serikali imetoa Tshs. Bilioni 196.8 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya elimu na kufanikisha kujenga shule mpya 157 pamoja na madarasa zaidi ya elfu 30.

Amebainisha hayo leo tarehe 06 Juni, 2026 katika Tamasha maalumu lililofanyika katika uwanja wa CCM Kirumba lililowakutanisha zaidi ya walimu 4000 kutoka kwenye shule binafsi na za Serikali za Awali, Msingi na Sekondari kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.

Aidha, amebainisha juhudi za serikali katika kuendelea kuboresha maisha ya walimu kwamba kwa kipindi cha muda mfupi Tshs. Bilioni 2.5 zimelipwa kama mapunjo ya mshahara kwa walimu.

Aidha, Mhe. Mtanda amewapongeza walimu 1170  wa shule za msingi na 393 wa sekondari kwa kufanikisha kuongeza ufaulu kwa wanafunzi katika matokeo ya darasa la saba hadi 92% na 90% kwenye matokeo ya kidato cha pili na nne.

Aidha, katika kuhakikisha anawajenga walimu wake kuwa na ari ya kufundisha siku za hivi karibuni atakutana na walimu
256 wenye madeni chechefu ambayo yanawafanya wakose utulivu wa akili ili kujadiliana nao namna ya kumaliza madeni hayo na kurudi kwenye utulivu.

Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe. Amiri Mkalipa ametumia wasaa huo kuwapongeza kwa ujumla wao walimu wote zaidi ya elfu nne kutoka katika shule za msingi na sekondari za serikali na binafsi wilayani humo kwa kuweka juhudi kubwa katika kuwafundisha watoto na kuongeza ufaulu.

kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Bi. Ummy Wayayu amewashukuru walimu wa Awali, Msingi na Sekondari kwa kupandisha ufaulu kwa wanafunzi mfululizo 2023, 2024 na 2025 kwenye matokeo ya Upimaji, kumaliza elimu msingi na sekondari pamoja na kidato cha sita.

Aidha, amebainisha kuwa manispaa hiyo ina jumla ya shule za msingi 167 (84 serikali na 83 binafsi) na shule za sekondari 63 (37 sekondari na 26 binafsi) na ametumia wasaa huo kumshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali walimu kwenye maslahi yao.


Post a Comment

0 Comments