TAKUKURU YAMREJESHA NCHINI MTUHUMIWA WA UTAPELI WA BILIONI 1.6

 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Kinondoni imemrejesha nchini mtuhumiwa Stephane Ngole maarufu kama Thomas Maweja, mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya STECA EXPORT COMPANY LIMITED, aliyekuwa akisakwa kwa tuhuma za makosa ya kifedha baada ya kutoroka nchini tangu mwaka 2023.

Akizungumza Mei 22, 2026 katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere International Airport Dar es salaam, Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Kinondoni, Christian Nyakizes, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa mjini Entebbe nchini Uganda mwezi Aprili 2026 kupitia operesheni maalum iliyohusisha ushirikiano wa vyombo vya uchunguzi vya ndani pamoja na Interpol.

Ngole anakabiliwa na mashtaka katika Shauri la Jinai Na. 12/2023 linaloendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akishtakiwa pamoja na wenzake kwa makosa ya kughushi nyaraka, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu pamoja na utakatishaji wa fedha haramu.

Kwa mujibu wa TAKUKURU, washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia zaidi ya Dola 678,810 za Marekani, sawa na takribani Shilingi bilioni 1.6, kupitia biashara ya tani 110 za madini ya shaba. Inadaiwa kuwa mwaka 2022 walipaswa kusafirisha mzigo wa madini hayo nje ya nchi, lakini badala yake makontena matano yaliyosafirishwa yalibainika kuwa yamejazwa chupa tupu za vinywaji.

TAKUKURU ilisema mtuhumiwa huyo, ambaye ni raia wa Democratic Republic of the Congo, alitoweka mara baada ya uchunguzi dhidi ya washitakiwa wenzake kukamilika na kufikishwa mahakamani. Aidha, alifuatiliwa katika mataifa mbalimbali kabla ya hatimaye kutiwa mbaroni nchini Uganda.

Mamlaka hiyo imeeleza kuwa baada ya kukamilika kwa taratibu zote za kisheria, mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani kuunganishwa rasmi na washitakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo.


 

Post a Comment

0 Comments