Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda ameipa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela muda wa miezi mitatu kuhakikisha inalipa madeni yote ya fidia kwa wananchi waliopisha maeneo ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mhe. Mtanda ametoa agizo hilo leo Mei 12, 2026 wakati wa mkutano wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi uliofanyika katika eneo la Kanisa Katoliki, Mtaa wa Lugeye, Kata ya Sangabuye, Manispaa ya Ilemela.
Ametoa pole kwa wananchi wanaodai fidia tangu mwaka 2022 kutokana na mradi wa viwanja vya Nyafula pamoja na maeneo ya machinjio, akisisitiza kuwa serikali haitaruhusu wananchi kunyimwa haki zao.
RC Mtanda amesema mikutano ya kutatua migogoro hiyo itaendelea kufanyika ili kuhakikisha wananchi wote wanaostahili wanalipwa fidia zao kwa wakati.
Aidha, amesisitiza kuwa hakuna mradi wowote utakaoendelea bila wananchi kulipwa fidia kwanza, huku akitaka malipo ya fidia kwa wananchi wa Nyafula kuanza kutolewa ndani ya kipindi cha Mei hadi Julai mwaka huu.
Katika madai hayo, wananchi wa maeneo ya Lugeye, Igalagala na Ikaku wanadai zaidi ya shilingi milioni 84, huku deni lote la fidia katika mradi wa Nyafula likifikia zaidi ya shilingi milioni 285.
Akisoma taarifa ya mradi huo, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Goodluck Lukandiza amesema mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi ulitekelezwa katika kata za Sangabuye, Lugeye, Nyafula na Igalagala baada ya halmashauri kupata mkopo wa zaidi ya shilingi bilioni 3.5 kutoka Wizara ya Ardhi.
Amesema wananchi 1,492 walifanyiwa uthamini wa fidia wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 5.3, huku deni lililobaki katika mradi wa Nyafula likiwa ni shilingi milioni 285, na kuongeza kuwa halmashauri inaendelea kushughulikia changamoto zote zinazojitokeza ili kuhakikisha wananchi wanapata haki zao.


.jpeg)


0 Comments