SERIKALI imesema kiasi cha tani milioni 12- 17 za taka ngumu huzalishwa hapa nchini kila mwaka ambapo asilimia ndogo ya taka hizo ndizo hurejelezwa.
Kauli hiyo imetolewa Mei 11, 2026 Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, 2026.
Mhe. Masauni amesema uzalishaji wa taka ngumu unatarajia kuongezeka hadi kufikia tani milioni 30-60 kwa mwaka ifikapo mwaka 2050 ambapo asilimia 60- 75 ni taka oza na asilimia 10-15 ni taka rejelezi.
Waziri Masauni ameyasema hayo wakati akitoa Tamko la Serikali kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari katika Ofisi za Makamu wa Rais Luthuli, Jijini Dar es Salaam, Mei 11, 2026.
‘Kila Mtanzania anapaswa kuchukua hatua sasa ili kuhakikisha kuwa maendeleo tunayoyapata hayaathiri mazingira na maisha ya vizazi vijavyo na kuonesha dhamira thabiti kwa vitendo kuhusu ajenda ya hifadhi ya Mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi”.
Mhandisi Masauni amesema kupitia sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 na mkakati wa utekelezaji wake, Serikali inaendelea kuimarisha juhudi katika uhifadhi wa misitu kupitia kampeni endelevu za upandaji miti, kukuza matumizi ya nishati safi na mbadala. Mhe. Masauni ameeleza kuwa, hivi karibuni Tanzania itaanza rasmi utekelezaji Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 ambapo Nguzo ya Tatu inahusu Uhifadhi wa Mazingira na Ustahimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi.
Kwa mujibu wa Mhandisi Masauni, ameeleza kuwa maadhimisho ya siku ya Mazingira duniani, yatafikia, kilele chake tarehe 5 Juni, 2026, hivyo Serikali inaendelea kuwahamasisha wananchi kushiriki shughuli mbalimbali ikiwemo upandaji na utunzaji miti pamoja na kuongeza kasi katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Waziri Masauni amesema shughuli mbalimbali za matukio zilizopangwa kufanyika katika maadhimisho hayo ni pamoja na Ushiriki wa viongozi na wananchi katika shughuli za kielelezo za upandaji miti na usafi wa mazingira katika Majiji ya (Arusha, Dar es salaam, Dodoma Mbeya, Mwanza na Tanga).
Aidha shughuli nyingine iliyopangwa ni pamoja na Kongamano la Kisayansi na Utafiti wa Mazingira ambayo ni mojawapo ya shughuli za maadhimisho ya Miaka 40 ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na uzinduzi wa Kongamano la Wadau wa Mazingira.
Aidha amesema shughuli nyingine iliyopangwa ni uzinduzi wa Kituo cha Afrika cha Vijana cha Kuwajengea Uwezo kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na hivyo kuboresha ushiriki wao katika usimamizi na majadiliano katika majukwaa ya kimataifa .
Sanjari tukio hilo kutakuwa na Uzinduzi wa Kituo cha Majanga yanayosababishwa na ‘Mabadiliko ya Tabianchi - Afrika. Kituo hiki kimefunguliwa nchini Tanzania mara baada ya kupata ridhaa ya Vikao ya Umoja wa Mataifa vinavyoshughulika na Masuala ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi.
Katika mkutano huo, Waziri Masauni aliongozana na Menejimenti ya Ofisi hiyo wakiongozwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, Naibu Katibu Mkuu ( Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Balozi Baraka Luvanda, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kituo chaTaifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC), Bi. Kathryn Kigaraba.
Kauli Mbiu ya Kimataifa ya Siku ya Mazingira Duniani, 2026 inasema "Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kwa Vitendo" ambapo juhudi zinaelekezwa katika kuongeza kasi na juhudi za kupunguza uzalishaji wa gesijoto, kukuza matumizi ya nishati mbadala, na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Wakati kauli mbiu ya Kitaifa inasema ”Dira 2050 Tuwajibike Kukijanisha Tanzania”
MWISHO
.jpeg)
0 Comments