MBETO AWATAKA WANASIASA, WACHAMBUZI NA WANATAALUMA KULINDA MASLAHI YA TAIFA

Na Mwandishi  Wetu, Zanzibar 

Chama Cha Mapinduzi  kimewataka Viongozi Wastaafu, Wanataaluma, Wasomi Wabobezi na Wachambuzi  wa Masuala ya Kisiasa ,Kijamii na Kiuchumi  , kutambua  dhima ya  gharama  ya kujenga  Taifa ni ghali kuliko  hasara ya kulibomoa.

Pia kimetaja  ulimi wa binadamu unapototoa maneno bila tafakuri ni sawa na kuchezea upanga wenye makali   au  kuwasha moto  unaosambaa na kuteketeteza  Misitu ,Mbuga na Nyika.

Maneno hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC  Zanzibar, Idara ya Itikadi  Uenezi na Mafunzo , Khamis Mbeto Khamis  aliyewataka Watanzania kujua thamani  ya  Umoja wao  kuliko  hasara ya kutoa maneno yanayopandikiza chuki , hasama na upasi katika jamii . Mbeto alisema wananchi,  wastaafu, wasomi, wachambuzi na wanataaluma  wanaopaswa kuwa wa kwanza kuitakia mema Tanzania   na kwamba hata  watakaolifikisha miaka sitini  ijayo huku Taifa likiwa moja ni Watanzania wenyewe.

Akizungumza bila kutaja majina ya watu ,vyeo au Taasisi zao, Mbeto alisema  hivi karibuni kumezuka  tabia ya  baadhi ya watu   kutamka maneno bila kupima athari na faida zake  katika jamii yenye  watu waungwana .

"Tabia ya baadhi  ya viongozi  Wastaafu   kutoa maneno makali bila kuyapima ni hatari . Pia kuna  baadhi ya Wasomi na  Wanataaluma wanaoheshimika  hutamka maneno ya  kuogofya. Wajue tu maneno makali hubomoa badala ya  kujenga nchi  "  Alisema  Mbeto .

Katibu huyo Mwenezi  alisema ipo haja ya kujadiliana mambo kwa kufuata taratibu zinazofaa ambazo haziachi athari katika jamii lakini pia si uungwana watu wazima wakawa na sifa ya kusemasema hovyo kila uchao ili kutaka sifa ya utukufu . 

"Ni kosa mtu kufikiri yatakapozuka majanga  au machafuko ana uhakika wa kubaki salama. Fujo, ghasia na vurugu hazina macho wala masikio. Huwadhuru matajiri, masikini, viongozi na raia wema  wasio na hatia bila kutarajia"Aliasa.

Aidha Katibu Mwenezi  huyo alisema hakuna  gumu lisiloweza kuzungumzika na kumalizwa kwa njia za kiungwana , hivyo  aliwashauri  viongozi wastaafu wa ngazi zote, Wanataaluma na Wasomi Wabobezi ,  maneno yao yajiegemeze zaidi katika kujenga na  kulinda umoja wa Kitaifa.

"Wapo baadhi ya wenzetu wanataka kutumia fujo na  vurugu kama mtaji wa kushika madaraka. Huwezi kupata utawala kwa mbinu  hizo batili. Njia pekee  inayokubalika ni  demokrasia ya  uchaguzi  ili kushika uongozi badala ya kususia  "Alikumbusha Mbeto

Katibu  huyo Mwenezi  alisema kuna baadhi ya wanasiasa  wanapohutubia kwenye majukwaa mbele ya wananchi,hawataki kuzingatia mantiki  ya kisheria inavyosema badala yake huvuka mipaka huku wakitamka na kueneza shari.

"Siasa za kuhubiri shari zimeyavuruga Mataifa mengi hususan  Barani Afrika . Maneno makali yasio na vipimo yamevuruga umoja , Amani  na kusibabisha mauaji  ,Vita na Umwagajidamu" Alisisitiza  Mbeto


 

Post a Comment

0 Comments