Na Mwandishi wetu
Kampuni ya DP World imesema uwekezaji katika miundombinu na uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam umeanza kuzaa matokeo makubwa, ukionekana kupitia ongezeko la kasi la mizigo katika mwaka mmoja tu.
Takwimu zinaonesha kuwa makontena (TEU) yameongezeka kutoka 209,238 mwaka 2024 hadi 323,837 mwaka 2025, sawa na ukuaji wa asilimia 55. Mizigo ya jumla (general cargo) imeongezeka kutoka tani milioni 1.78 hadi tani milioni 2.23, ikiwa ni ukuaji wa asilimia 25, huku mizigo ya bulk ikikua kwa asilimia 22 na kufikia tani milioni 3.89.
Magari (RoRo) yaliyohudumiwa pia yameongezeka kwa asilimia 20 kutoka 187,500 hadi 224,854, yakionesha kuimarika kwa biashara ya magari na vifaa vikubwa.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Uhusiano wa DP World Tanzania, Elitunu Malamia, rekodi kadhaa zimewekwa, ikiwemo kushughulikia magari 30,442 na makontena 43,803 ndani ya mwezi Machi 2026, kiwango cha juu kuwahi kufikiwa kwa mwezi mmoja.
Alisema ukuaji huo unatokana na maboresho ya vifaa, mifumo ya kidijitali na ongezeko la ufanisi wa operesheni bandarini.
Mwelekeo huo unaonesha kuwa uwekezaji katika bandari una athari ya moja kwa moja katika kupanua biashara, kupunguza gharama za usafirishaji na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara ya kikanda.

0 Comments