Dodoma
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amewataka wadau wa madini ya metali (base metals) kujipanga kimkakati na kuifanya sekta hiyo kuwa kichocheo kipya cha ukuaji wa uchumi wa viwanda nchini, akisisitiza kuwa usimamizi madhubuti wa rasilimali, uwekezaji katika teknolojia za kisasa, uongezaji thamani, pamoja na kuzingatia misingi ya uwajibikaji na uwazi ni nguzo kuu za kuongeza tija, thamani na ushindani wa madini hayo katika soko la madini hayo.
Amesema kuwa kupitia mbinu hizo, sekta ndogo ya madini ya metali ina uwezo mkubwa wa kufungua fursa za ajira, kuongeza mapato ya Taifa na kuimarisha mnyororo wa thamani wa viwanda, hivyo kuchangia kwa kiwango kikubwa katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi shindani na wa viwanda endelevu.
Amesema hayo leo Aprili 20, 2026 wakati akizungumza katika kikao na wadau wa Tanzania Base Metal Association (TBMA) kilichofanyika katika Ukumbi wa Tume ya Madini Jijini Dodoma, ambako amesema Serikali ina dhamira ya dhati ya kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji ili sekta hiyo iweze kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
“Mwelekeo wetu ni kuhakikisha sekta ndogo ya madini ya metali inakuwa na mchango mkubwa zaidi katika uchumi. Tutahakikisha changamoto zinazowakabili wadau zinapatiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu,” amesisitiza Mavunde.
Mhe. Mavunde ametumia kikao hicho kusikiliza na kupokea changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji wa madini ya metali, ikiwemo masuala ya miundombinu na masoko, huku akiagiza uanzishwaji wa Kituo cha Madini eneo la Mlongo-Kyerwa mahususi kwa ajili ya wachimbaji wa madini bati (tin) huku akiahidi kuzifanyia kazi kwa haraka.




0 Comments