ALIYETOKA JELA AKUTWA AMEUWAWA MOROGORO

Na Ally Mandai,Morogoro.

Mwanaume mmoja aliyefahamika kwa jina la Jafari, mkazi wa eneo la Kilimahewa katika kata ya Mafisa, Manispaa ya Morogoro, ameuawa kikatili na watu wasiojulikana, huku mwili wake ukikutwa umetupwa kwenye kichaka karibu na eneo la kutupia taka, tukio lililozua hofu na taharuki miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.

Kwa mujibu wa mashuhuda, akiwemo mkazi wa eneo hilo Hellen Yohana, mwili wa marehemu uligunduliwa majira ya asubuhi wakati wananchi wakielekea kwenye shughuli zao za kila siku. Amesema walikuta mwili huo ukiwa umelala chini na ukiwa na majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili, hali iliyoashiria kuwa huenda aliuawa kikatili kabla ya kutupwa eneo hilo.

Akizungumzia tukio hilo, Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kilimahewa, Gresford Magodi, amesema kuwa marehemu alikuwa ametoka gerezani siku chache zilizopita. Ameeleza kuwa baada ya kurejea uraiani, kulikuwa na taarifa zinazodai kuwa alikuwa akijihusisha na vitendo vya wizi, jambo ambalo baadhi ya wananchi wanahisi linaweza kuwa limehusika na tukio hilo la mauaji, ingawa hakuna uthibitisho rasmi uliotolewa hadi sasa.

Wananchi wa Kilimahewa wameeleza kushtushwa na tukio hilo na kutoa wito kwa vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini waliohusika na kuhakikisha wanachukuliwa hatua za kisheria. Aidha, wameitaka jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake kufuata taratibu za kisheria pale wanapokumbana na vitendo vya uhalifu.

Kwa sasa, Darasa Huru Media inaendelea kufanya juhudi za kuwasiliana na Jeshi la Polisi pamoja na mamlaka husika ili kupata taarifa rasmi na za kina zaidi kuhusu tukio hilo, huku uchunguzi ukiendelea kubaini ukweli wa kilichotokea.

KAMA UNA TAARIFA YOYOTE WASILIANA NASI KUPITIA NAMBA 0654414804. 


 

Post a Comment

0 Comments