MKOA WA PWANI UMEJIPANGA KUPOKEA MWENGE WA UHURU

Mkoa wa Pwani umekamilisha maandalizi na umejipanga vyema kupokea Mwenge wa Uhuru utakaowasili Aprili 18, 2026, ukitokea Mkoa wa Dar es Salaam.

Hayo yameelezwa leo, Aprili 16, 2026, na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi mdogo wa mikutano uliopo ofisini kwake, Kibaha mkoani humo.

Amesema mapokezi hayo yatafanyika katika Wilaya ya Bagamoyo, Kata ya Mapinga, katika viwanja vya Shule ya Msingi Mtambani. Aidha, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki tukio hilo muhimu la kihistoria.

Aliongeza kuwa Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika halmashauri zote tisa za mkoa huo, ukiambatana na shughuli mbalimbali za maendeleo, zikiwemo uwekaji wa mawe ya msingi, ukaguzi na uziduzi wa miradi inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.

Kaulimbiu ya mwaka huu inasema: “Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo.” Kaulimbiu hiyo inahimiza ushirikiano, kudumisha amani na kufanya kazi kwa bidii ili kufanikisha maendeleo endelevu ya Taifa.

Aidha, amewakaribisha wananchi wote wa Mkoa wa Pwani na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki mapokezi ya Mwenge wa Uhuru pamoja na kushiriki kikamilifu katika shughuli zote zitakazofanyika katika kipindi chote cha mbio za Mwenge mkoani humo.



Post a Comment

0 Comments