Na Ally Mandai,Tabora.
Mwanamke mmoja mjane mkazi wa Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, Fatma Nassoro amepoteza zaidi ya shilingi milioni 40 baada ya kutapeliwa na watu wanaodaiwa kujifanya mawakala wa huduma ya LIPA NAMBA, fedha ambazo ni sehemu ya mirathi aliyoachiwa na marehemu mume wake.
Inadaiwa kuwa watuhumiwa hao walifika katika eneo la biashara la Fatma wakijitambulisha kuwa ni watoa huduma wanaotaka kumsaidia kuunganisha mfumo wa malipo ya kielektroniki katika biashara yake.
Kupitia ujanja huo, walifanikiwa kupata namba yake ya siri ya miamala na baadaye kuhamisha fedha zote kutoka kwenye akaunti yake bila yeye kutambua mara moja kilichokuwa kinaendelea.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa tayari limewakamata watu watano wanaohusishwa na utapeli huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora,SACP Richard Abwao, amesema watuhumiwa hao walikamatwa katika mji wa Babati mkoani Manyara walipokuwa wakijaribu kutoroka baada ya kutekeleza uhalifu huo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, amelielekeza Jeshi la Polisi kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa kwa haraka kwa mwanamke huyo pamoja na kuchukuliwa hatua kali za kisheria dhidi ya watuhumiwa hao ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo.
Wakati huo huo, Kampuni za Yas na Mixx zimelaani tukio hilo na kutoa tahadhari kwa wananchi kutowahi kutoa namba zao za siri kwa mtu yeyote, huku zikisisitiza kuwa wateja wanapaswa kuripoti mara moja vitendo vya watu wanaojifanya mawakala wa huduma za kifedha.

0 Comments