Mamlaka ya
Udhibiti Usafiri Ardhini, LATRA, imeonya watoa huduma za usafiri nchini
kuacha mara moja kupandisha nauli kiholela bila kufuata taratibu za
kisheria.
Onyo hilo linakuja wakati baadhi ya waendeshaji wa
mabasi na daladala wakianza kuongeza nauli wakihofia kupanda kwa gharama
za uendeshaji, hali inayowaathiri wananchi, hasa wa kipato cha chini na
wanafunzi.
Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Habib Suluo, alisema
mamlaka hiyo inatambua changamoto za sekta hiyo, lakini mabadiliko ya
nauli lazima yafanyike kwa kufuata sheria na kanuni zilizowekwa.
“Hatutaruhusu ongezeko holela la nauli. Lazima utaratibu ufuatwe ili kulinda maslahi ya wananchi,” alisema.
Alisema LATRA itaitisha kikao cha wadau Aprili 8 jijini Dar es Salaam kujadili hali hiyo na kupata suluhisho la pamoja.
Kwa
mujibu wa sheria, nauli hupangwa na LATRA, kuidhinishwa na Bodi ya
Wakurugenzi na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali kabla ya kuanza
kutumika rasmi baada ya siku 14.
0 Comments