Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, amewataka Watendaji wa Kata, Maafisa Maendeleo ya Jamii, Wenyeviti wa Kamati za Mikopo za Kata kusimamia kwa uadilifu na weledi mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri, ili iweze kuwafikia wananchi wenye sifa na kuleta maendeleo ya kweli katika jamii.
Kauli hiyo ameitoa Leo tarehe 28 April katika kikao kazi kilichoandaliwa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kilichofanyika katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam
Mhe. Mpogolo amesema mafunzo yaliyotolewa na Benki ya CRDB kwa watendaji hao yataongeza uwezo wa usimamizi wa mikopo hiyo, kuboresha utendaji kazi na kusaidia kuongeza idadi ya vikundi vitakavyonufaika na mpango huo.
Amesema kupitia elimu hiyo, watendaji wataweza kusimamia mchakato wa utoaji wa mikopo kwa ufanisi zaidi, kuondoa vikwazo visivyo vya lazima na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata fursa hiyo.
Aidha, ameishukuru Benki ya CRDB kwa ushirikiano wake katika utekelezaji wa mpango huo, huku akiitaka kuhakikisha mikopo inatolewa kwa wakati kwa vikundi vyote vilivyokidhi vigezo na masharti.
" utolewaji wa mikopo kwa wakati utawezesha vikundi kuanza au kuendeleza shughuli zao za kiuchumi kwa wakati, kuongeza uzalishaji na kuinua kipato cha wananchi." amesisitiza DC MPOGOLO
Pia ameielekeza Idara ya Maendeleo ya Jamii kuanzisha dawati la malalamiko litakalowezesha wananchi na vikundi kuwasilisha changamoto zao na kupata ufumbuzi wa haraka.





0 Comments