TAKUKURU YAREJESHA TABASAMU HOSPITALI KINONDONI,YATOA MASHINE NA VIFAA TIBA KWA WATOTO NJITI

 Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Crispin Chalamila, amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na sekta ya afya nchini kwa lengo la kuboresha huduma na kuokoa maisha ya wananchi, hususan watoto wachanga.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa tiba katika Hospitali ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Bw. Chalamila alianza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha kukutana salama kutekeleza jukumu hilo muhimu la kijamii.

“Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana hapa leo tukiwa wazima kwa ajili ya kutekeleza jukumu hili,” alisema Bw. Chalamila.

Alitumia fursa hiyo kuushukuru uongozi wa Hospitali ya Manispaa ya Kinondoni kwa mapokezi mazuri na maandalizi ya hafla hiyo, akisema yalizidi matarajio yao tangu walipowasili.

“Nawashukuru sana uongozi wa hospitali kwa mapokezi na maandalizi mazuri ya tukio hili, kwa kweli hatukutarajia maandalizi ya kiwango hiki,” aliongeza.

Bw. Chalamila alieleza kuwa ushirikiano kati ya TAKUKURU na hospitali hiyo umekuwa wa manufaa kwa pande zote mbili, huku kila upande ukitoa elimu katika maeneo yake ya kitaaluma.

“Tumekuwa tukishirikiana kwa karibu, ninyi mkitoa elimu ya afya kwa watumishi wetu na sisi tukitoa elimu ya kupambana na rushwa, na ushirikiano huu umezaa matunda,” alisema.

Aidha, alieleza kuridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya hospitali hiyo unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni tano, akibainisha kuwa hakuna dosari zilizobainika hadi sasa.

“Kwa taarifa tulizonazo, hakuna dosari yoyote katika utekelezaji wa mradi huu, na hilo ni jambo la kupongezwa sana,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, alimshukuru Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kwa kushiriki katika hafla hiyo na kuipa uzito unaostahili, pamoja na Mbunge wa Jimbo la Kawe ambaye alituma salamu za kuunga mkono tukio hilo licha ya kutokuwepo.

Akifafanua majukumu ya TAKUKURU, Bw. Chalamila alisema taasisi hiyo inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa Sura ya 329, ambayo inahusisha kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa.

“Katika kuzuia rushwa tunafanya tafiti, uchambuzi wa mifumo na kutoa elimu kwa jamii, na katika kupambana tunachunguza na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika wa vitendo vya rushwa,” alisema.

Aliongeza kuwa TAKUKURU ina jumla ya ofisi 145 nchini, ikiwa imeenea katika mikoa 28 na wilaya 111, huku mkoa wa Dar es Salaam ukiwa na ofisi tatu tofauti kutokana na ukubwa na umuhimu wake.

Kuhusu msaada uliotolewa, Bw. Chalamila alisema unahusisha mashine mbili muhimu kwa ajili ya kuwahudumia watoto wachanga, ambazo ni mashine ya kuwapatia joto watoto njiti (Infant Incubator) na mashine ya tiba ya mwanga kwa watoto wenye homa ya manjano (Phototherapy Machine).

“Tumefanya utafiti mdogo na kubaini kuwa kuna ongezeko la watoto njiti na wenye uzito mdogo, hali inayochangia vifo vya watoto kutokana na ukosefu wa vifaa maalum kama hivi tulivyovileta leo,” alieleza.

Alisema licha ya TAKUKURU kutofanya biashara yoyote, watumishi wake wamekuwa wakichangishana kwa hiari ili kusaidia jamii, ikiwa ni sehemu ya uzalendo na uwajibikaji wa kijamii.

“Sisi ni watumishi wa umma lakini pia ni wazazi na raia wa Tanzania, tuna wajibu wa kushiriki katika kuboresha huduma za afya,” alisema.

Bw. Chalamila alibainisha kuwa hatua hiyo inaunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuboresha sekta ya afya nchini.

“Serikali imefanya kazi kubwa sana katika kuboresha huduma za afya, ikiwemo ujenzi wa hospitali na vituo vya afya pamoja na kuimarisha huduma za rufaa,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa TAKUKURU imelenga kusambaza vifaa hivyo katika hospitali za rufaa za mikoa, na hadi sasa tayari wamefikia hospitali 18, huku zoezi hilo likiendelea katika maeneo mbalimbali nchini.






Post a Comment

0 Comments