MGODI WA KIHISTORIA WA NIOBIUM KUJENGWA MKOANI MBEYA

 Tanzania imeingia hatua muhimu ya kuimarisha biashara na Marekani baada ya Serikali na Panda Hill Tanzania Limited kusaini mkataba wa makubaliano ya kuendeleza Mradi wa Niobium wa Panda Hill, hatua inayolenga kuifanya Mbeya kuwa kitovu cha uzalishaji na usindikaji wa madini mkakati.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Madini Mheshimiwa Anthony Mavunde alisema mradi huo ni wa uzalishaji wa madini adimu ambayo hayapatikani kila mahali duniani, na kwamba Tanzania inalenga kuchukua nafasi ya kipekee katika soko la kimataifa la niobium kupitia mradi huo. Alisema soko la dunia kwa sasa linatawaliwa na wazalishaji wachache wakubwa, na Panda Hill itaiweka Tanzania kwenye ramani ya wazalishaji wakuu duniani.

Mheshimiwa Mavunde alieleza kuwa mzalishaji mkubwa duniani yupo Brazil na huzalisha takriban asilimia 80 ya mahitaji ya dunia, mzalishaji wa pili naye yupo Brazil na huzalisha takriban asilimia 11, huku Canada ikichangia takriban asilimia 6. Kupitia Panda Hill, alisema Tanzania inalenga kuwa mzalishaji wa nne duniani kwa kuchangia takriban asilimia 4 ya mahitaji ya dunia, na uzalishaji unaolengwa kufikia takriban tani 100,000 kwa mwaka.

Katika kusisitiza mwelekeo wa Serikali, Waziri Mavunde alisema dira ya maendeleo ya 2025-2050 na maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yanalenga kuhakikisha madini yanaongezewa thamani hapa hapa nchini ili manufaa yawe makubwa kwa wananchi. Alisema Tanzania inaenda zaidi ya uchimbaji wa kawaida kwa kujenga uwezo wa ndani wa kuchakata na kuzalisha bidhaa za viwandani zenye thamani kubwa.

Mradi huo unahusisha niobium, madini ya kimkakati inayotumika kuongeza uimara wa chuma na kutengeneza aloi za utendaji.


Post a Comment

0 Comments