MAMA MARIAM MWINYI AWATAKA JAMII KUWASAIDIA WAZEE NA WATOTO MAYATIMA

 Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti na Msarifu wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation, Mama Mariam Mwinyi, ameisisitiza jamii kuendelea kuwasaidia wazee wasiojiweza na watoto mayatima ili nao waishi maisha bora na katika mazingira salama.

Tamko hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Zawadi Amour Nassor, kwa niaba ya Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi, leo tarehe 12 Machi 2026 alipomuwakilisha katika hafla ya kukabidhi sadaka ya futari kwa wazee wasiojiweza wanaotunzwa katika Kituo cha Wazee Kifumbikai na Kituo cha Mayatima kilichopo Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Amefahamisha kuwa jamii ina wajibu muhimu wa kuwalea na kuwatunza wazee, kwani kuna fadhila kubwa kwa Mwenyezi Mungu, sambamba na kuwa ni jambo jema baada ya wazee hao kulitumikia Taifa kwa juhudi kubwa.

Mama Mariam Mwinyi amesema Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation itaendelea kuunga mkono dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuendelea kuwatunza wazee na mayatima, na kutoa wito kwa taasisi na wadau wengine kujitokeza kuwasaidia.

Wakitoa salamu kwa niaba ya wazee, Mzee Saidi Bakari na Bi. Subira Omar Muhammed kwa pamoja wamemshukuru Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi kwa kuwajali na kuonesha upendo mkubwa kwao, pamoja na kuendeleza utaratibu huo kila mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Naye Mkuu wa Kituo cha Kutunzia Wazee, Ndg. Suleiman Muhidan Assaa, amemshukuru Mama Mariam Mwinyi kupitia taasisi yake ya Zanzibar Maisha Bora Foundation kwa kuendelea kuwapatia sadaka ya futari wazee hao, hatua aliyoielezea kuwa ni msaada mkubwa unaowafanya wazee hao kuishi kwa furaha na matumaini.

Ugawaji huo wa sadaka ya futari pia umefanyika katika Kituo cha Kulelea na Kutunza Watoto Mayatima cha Daarul Ahbaab kilichopo Micheweni, chenye watoto yatima 45.
Mlezi Mkuu wa kituo hicho, Ndg. Khamis Abdalla, naye amemshukuru Mke wa Rais wa Zanzibar kwa kuonesha utu, imani na kuwajali watoto mayatima, pamoja na kuendeleza juhudi zake za kuunga mkono wadau kw kuwalea na kuwatunza watoto hao.


Post a Comment

0 Comments