DC KALLI AAGIZA MATUMIZI BORA YA ARDHI KUMALIZA MIGOGORO LONGIDO

Na Mwandishi wetu,Longido

Mkuu wa Wilaya ya Longido, Salum Kalli, amewataka Watendaji wa Kata na Vijiji kuhakikisha wanatengeneza na kusimamia matumizi bora ya ardhi ili kumaliza migogoro ya ardhi katika maeneo yao.

Mhe. Kalli ametoa kauli hiyo leo Machi 4, 2026, katika kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na Watendaji wa Vijiji na Kata kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri J.K. Nyerere.

“Ardhi inatugombanisha sana; ardhi ni shida. Naomba watendaji wa vijiji na kata mtengeneze matumizi bora ya ardhi ili kumaliza migogoro ya wananchi,” amesema Mhe. Kalli.

Ameeleza kuwa takribani asilimia 50 ya migogoro ya wananchi inatokana na ardhi, hivyo amewataka viongozi hao kutafuta na kusimamia ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo.

Amesisitiza kuwa iwapo suala la usimamizi wa ardhi litasimamiwa kwa umakini, migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Longido itapungua au kumalizika kabisa.

Aidha, amewaelekeza viongozi hao kufanya kazi kwa kuwafikia wananchi moja kwa moja na kutatua kero zao badala ya kukaa ofisini.


 

Post a Comment

0 Comments