Na Ally Mandai.
Maswali yaliyoibuka kwa mashabiki kuhusu wapi itapigwa Dabi ya Dar es Salaam kati ya Azam FC na Yanga katika Ligi Kuu hatimaye yamepatiwa majibu rasmi, kufuatia kufungwa kwa Uwanja wa Benjamin Mkapa kupisha maboresho makubwa kuelekea Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2027.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, pambano hilo kubwa la watani wa jadi litakalochezwa Machi 15, 2026 sasa litafanyika katika Uwanja wa Azam Complex, uliopo Chamazi, jijini Dar es Salaam.
Azam FC watakuwa wenyeji wa mchezo huo unaotarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi wa soka nchini.
Akizungumza na vyombo vya habari, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Azam FC, Thabit Zakaria maarufu kama ‘Zaka Zakazi’, alithibitisha kuwa mchezo huo wa mzunguko wa kwanza wa ligi dhidi ya Yanga utafanyika Azam Complex badala ya Uwanja wa Mkapa kama ilivyozoeleka kwa mechi nyingi kubwa.
“Mechi hiyo itachezwa hapa nyumbani Azam Complex na siyo Mkapa kama ilivyozoeleka. Tunawakaribisha sana mashabiki waje kushuhudia mchezo mkubwa na wa kuvutia,” alisema Zaka Zakazi.
Dabi hiyo inatarajiwa kuwa na ushindani mkali, huku kila timu ikisaka pointi muhimu katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
TANGAZA NASI SASA,UWAFIKIE MAMILIONI YA WATEJA:Piga 0654414804.

0 Comments