Na Ally Mandai
Klabu ya Young Africans Sports Club (Yanga SC) leo imeadhimisha miaka 91 tangu kuanzishwa kwake, ikiendelea kuwa miongoni mwa klabu kongwe na zenye mafanikio makubwa katika soka la Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki.
Yanga ilianzishwa mwaka 1935 na tangu wakati huo imekuwa sehemu muhimu ya historia ya mpira wa miguu nchini. Katika kipindi cha zaidi ya miongo tisa, klabu hiyo imeshiriki na kutwaa mataji mbalimbali ya ndani ikiwemo Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na mashindano mengine ya kitaifa.
Mbali na mafanikio ya ndani, Yanga pia imekuwa mshiriki wa mara kwa mara katika mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), hatua iliyochangia kuitangaza Tanzania katika ramani ya soka la bara la Afrika.
Katika miaka ya karibuni, klabu hiyo imeendelea kufanya maboresho katika uendeshaji wake, ikiwemo kuimarisha mfumo wa uongozi, uwekezaji na maendeleo ya kikosi chake, hatua ambazo zimeongeza ushindani wake ndani na nje ya nchi.
Wakati ikiadhimisha miaka 91, Yanga pia inaendelea na maandalizi ya michezo yake ya kimataifa, ambapo kikosi hicho kinaendelea kujifua kwa ajili ya mchezo dhidi ya JS Kabylie unaotarajiwa kuchezwa Jumapili ya wiki hii. Maandalizi hayo yanafanyika chini ya benchi la ufundi kwa lengo la kuhakikisha timu inakuwa katika kiwango bora kuelekea mchezo huo muhimu.
Maadhimisho ya mwaka huu yanakuja sambamba na ratiba ya mashindano inayoendelea, huku klabu ikiingia mwaka wake wa 92 ikiwa na matarajio ya kuendeleza ushindani na mafanikio katika soka la ndani na kimataifa.




0 Comments