YANGA YAPIGWA MOROCCO,HESABU NGUMU NEW AMAAN COMPLEX

Na Ally Mandai.

Mchezo mgumu umemalizika rasmi nchini Morocco ambapo wenyeji FAR Rabat wamefanikiwa kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Yanga SC katika mwendelezo wa michezo ya Kundi B ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. 

Bao hilo pekee lililofungwa kwenye mchezo huo limekuwa pigo kubwa kwa Wananchi, ambao walihitaji angalau sare ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua inayofuata.

Katika mchezo huo, FAR Rabat walionekana kucheza kwa nidhamu kubwa, wakitumia vizuri faida ya uwanja wa nyumbani licha ya kukosekana kwa mashabiki wao. Yanga walijitahidi kupambana, wakitawala sehemu ya mchezo hasa kipindi cha pili, lakini umakini mdogo eneo la ulinzi na kushindwa kutumia nafasi walizozipata mbele ya lango kuligharimu kikosi hicho cha kocha wao.

Matokeo hayo yameifanya Yanga SC kushuka hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Kundi B, wakiwa na alama 5, hali inayoweka presha kubwa kuelekea mchezo wao wa mwisho wa hatua ya makundi. Kwa upande wa FAR Rabat, ushindi huo muhimu umeipandisha timu hiyo hadi nafasi ya pili kwa kujikusanyia alama 8, na sasa wamejiweka katika nafasi nzuri ya kupambana kufuzu robo fainali.

Sasa macho na masikio ya Wananchi yako kwenye mchezo wa mwisho ambapo Yanga SC wataikaribisha JS Kabylie katika Uwanja wa New Amaan Complex, mchezo ambao hauna nafasi ya makosa. Yanga wanalazimika kushinda mchezo huo na kusubiri matokeo ya mchezo mwingine ili kuhakikisha ndoto yao ya kusonga mbele inaendelea kuwa hai.

Wakati huo huo, FAR Rabat wanajiandaa kusafiri kuelekea Misri kuivaa Al Ahly, mchezo mwingine mgumu unaotarajiwa kuamua hatima ya Kundi B. Matokeo ya michezo hiyo miwili ya mwisho yataamua ni timu zipi zitavuka kwenda hatua ya robo fainali, huku presha ikiwa kubwa kwa kila upande.

Kwa sasa, hesabu zinaendelea, matumaini bado yapo, lakini ukweli unabaki pale pale Yanga hawana budi kupambana hadi dakika ya mwisho, kwani kosa dogo linaweza kuhitimisha safari yao mapema kwenye michuano ya msimu huu wa Ligi ya Mabingwa Afrika.






Post a Comment

0 Comments