Na Ally Mandai.
Msajili wa Vyama vya Michezo na Vilabu nchini, Bw. Abel M. Ngilangwa, amesema Katiba ya Klabu ya Simba iliyoidhinishwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Michezo imezingatia kikamilifu misingi ya Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa Sura ya 49 pamoja na kanuni zake.
Serikali, kupitia Baraza la Michezo la Taifa, imejiridhisha kuwa mchakato wa marekebisho umefanyika kwa kuzingatia matakwa ya kisheria, taratibu za usajili na kanuni za utawala bora. Hali hiyo inaifanya Katiba hii kuwa halali, thabiti na inayotekelezeka kwa manufaa ya klabu na wadau wake wote.
Kutokana na maelezo hayo, Ofisi ya Msajili imetoa idhini ya marekebisho hayo kwa sababu yanaendana na sheria na kanuni husika, yanaimarisha utawala bora, uwazi na uwajibikaji, yamezingatia ushauri wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali uliotolewa tarehe 12 Mei 2025, Yameondoa mikinzano iliyokuwapo katika Katiba ya mwaka 2018, Yameoanisha Katiba na matakwa ya taasisi mbalimbali za Serikali
Zaidi ya hayo, marekebisho haya yameoanisha matakwa ya taasisi za Serikali ikiwemo Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na Tume ya Ushindani, yamelinda maslahi ya wanachama huku yakiheshimu na kulinda uwekezaji uliokwisha kufanyika na utakaofanyika.
Marekebisho hayo hayalengi kunufaisha watu wachache bali kuweka uwiano wa haki kati ya wanachama na wawekezaji. Kupitia uidhinishaji huu, Serikali imeweka msingi thabiti wa usajili, umiliki na usimamizi wa mali kwa kuzingatia sheria za nchi, na hivyo kufungua ukurasa mpya wa utulivu, uwazi na maendeleo endelevu kwa klabu.



0 Comments