Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro na Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Polisi, Alhaji Dkt. Mussa Ali Mussa, amewataka Maafisa Tarafa mkoani humo kuhakikisha wanasimamia ipasavyo miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao ili ikamilike kwa wakati na kwa ubora unaohitajika kulingana na fedha iliyotolewa (value for Money).
Dkt. Mussa ametoa agizo hilo leo, Februari 4, 2026, wakati wa kikao chake na Maafisa Tarafa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo huku akisema kuwa, usimamizi wa miradi ni jukumu muhimu kwao katika kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na walengwa wanapata huduma za msingi kutokana na miradi hiyo.
".. Mmeacha wajibu huu mkubwa wa kuifuatilia miradi inayotekelezwa katika maeneo yenu.." amesisitiza Dkt. Mussa Ali Mussa
Aidha, amebainisha uwepo wa malalamiko mengi kuhusu baadhi ya Maafisa Tarafa kutokuwepo katika maeneo yao ya kazi na kuwataka kuacha tabia hiyo mara moja badala yake wawepo katika vituo vyao vya kazi muda wote wa kazi ili wananchi waweze kupata huduma za msingi kupitia wao bila usumbufu.
Katika hatua nyingine kiongozi huyo amekemea vikali tabia zisizofaa za baadhi ya Maafisa Tarafa kama ulevi na vitendo vingine visivyoendana na utumishi wa umma na kwamba mambo hayo yanaathiri vikubwa utendaji kazi na taswira ya utumishi wa umma.


0 Comments