Wanaharakati Ahmed Kombo na Joseph Yona wanatarajia kuanza ziara katika mikoa 15 nchini Tanzania kwa lengo la kuzungumza na vijana na kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kulinda na kudumisha amani ya taifa.
Wanaharakati hao wameiomba Serikali pamoja na wananchi wenye mapenzi mema kuwawezesha kufanikisha ziara hiyo ili waweze kuwafikia vijana wengi zaidi nchini.
Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwanaharakati Ahmed Kombo amesema kuwa ziara hiyo itaanza katika mikoa 15 ya awali kabla ya kuendelea na mikoa mingine.
Alisema hatua hiyo inalenga kukabiliana na jitihada za baadhi ya watu wasiolitakia taifa mema, wanaodaiwa kuwapotosha vijana kwa nia ya kuchafua amani ya nchi ambayo imejengwa kwa historia ndefu ya mshikamano na utulivu.
Wanaharakati hao wameiomba Serikali kuhakikisha amani ya nchi inaendelea kuwa thabiti ili kuondoa hofu na taharuki kwa wananchi.
Lengo kuu la ziara hiyo ni kutoa elimu kwa vijana kuhusu namna ya kutunza amani pamoja na kuwapa mbinu mbalimbali za kulinda nchi yao.
Kwa upande wake, Joseph Yona amesema kuwa vijana wanapaswa kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali ili kujikwamua kiuchumi.
Alibainisha kuwa Serikali imeweka kipaumbele katika kutoa mikopo kwa vijana, hivyo huu ni wakati muafaka kwa vijana kuitumia mikopo hiyo kuleta maendeleo binafsi na ya taifa kwa ujumla.
Aidha, vyombo vya ulinzi na usalama vimetakiwa kuendelea kushirikiana na wananchi katika kuhakikisha amani na usalama wa nchi unalindwa ipasavyo.

0 Comments