Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson Simon, amefungua mafunzo elekezi ya madiwani wa Halmashauri za Wilaya ya Kibaha na Chalinze yaliyofanyika leo Januari 15, 2026 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku tatu yanayoendeshwa na wakufunzi kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, Mhe. Nickson amewataka madiwani kuwa mabalozi wazuri wa usimamizi wa miradi ya maendeleo katika kata zao, akisisitiza uwajibikaji, matumizi ya takwimu na ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wa miradi.
Aidha, amesisitiza madiwani kutekeleza majukumu yao kwa lugha ya staha, kuepuka chuki na hasira, pamoja na kukosoa miradi badala ya watu, ili kuimarisha mahusiano kati ya viongozi, wataalam na wananchi.
Nickson pia, amewahimiza madiwani kujiepusha na tamaa ya mali ya umma, kukubali kukosoa na kukosolewa, kufanya kazi kwa ushirikiano na kutowabagua wananchi kwa misingi ya kisiasa.
Kwa upande wake, mkufunzi Bi. Esther Andrew Mdegipala kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, wamewahimiza madiwani kuwa wabunifu, kutumia kikamilifu vishikwambi walivyokabidhiwa, kuzingatia nidhamu, kuheshimu sheria na kutunza siri za uongozi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Mhe. Shomari Minshehe, ameishukuru Serikali kwa kuandaa mafunzo hayo akisema yatasaidia kuimarisha utawala bora, kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na kubaini mipaka ya majukumu baina ya madiwani na wataalam.
Naye Diwani wa Kata ya Kikongo, Bi. Halima Jongo, amesema mafunzo hayo yataimarisha ushirikiano miongoni mwa madiwani na kuwajengea uelewa mpana kuhusu nafasi yao katika kusimamia maendeleo ya wananchi.

0 Comments