Na Mwandishi Wetu,
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche, ametuhumiwa kutumia changamoto za kuwa mahabusu kwa Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, kwa manufaa yake binafsi.
Tuhuma hizo zinaeleza kuwa Heche anadaiwa kuzuia kwa makusudi jitihada za kumaliza kesi inayomkabili Lissu ili aendelee kubaki na ushawishi na madaraka makubwa ndani ya chama, ajijengee umaarufu wa kisiasa na kukusanya fedha kutoka ndani na nje ya nchi kwa kisingizio cha kuhamasisha mapambano ya kidemokrasia.
Tuhuma hizo zimetolewa na Habibu Mchange mwenyekiti wa MECIRA ambaye aliwahi kuwa mwanachama mwandamizi wa CHADEMA.
Kwa mujibu wa Mchange, hali ya sintofahamu imeibuka ndani ya chama ambapo kwa sasa Heche, Lema, Sugu na viongozi wengine hawazungumzi lugha moja baada ya kubaini kuwa Heche amewageuka wenzake na anataka kujimilikisha kila aina ya mjadala wa kisiasa kwa lengo la kujinufaisha kifedha.
Mchange anadai kuwa Heche anashirikiana na watu mbalimbali walioko ndani na nje ya serikali pamoja na chama chake ili kuhakikisha changamoto za kisiasa zinaendelea, ikiwemo kuzuiwa kwa ajenda ya maridhiano.
Kwa mtazamo wake, mkakati huo unamlenga kumpa Heche nafasi ya kuendelea kujijenga kisiasa na kiuchumi kupitia mgogoro unaoendelea.
Akizungumzia kwa upana zaidi, Mchange alisema kuwa viongozi wa vyama vya siasa, hususan wa upinzani, mara nyingi si wa kweli kwa wanachama wao kwani hutumia imani na matumaini waliyojengewa kama mtaji wa kujinufaisha binafsi.
Aliwataka wanachama wa vyama vya siasa kuwa makini, kutumia akili zao, na kuepuka kuingizwa kwenye migogoro inayochochewa kwa maslahi ya watu wachache walioko juu ya uongozi.
Katika kutoa mfano wa mahusiano ya kijamii yanayovuka mipaka ya vyama, Mchange alisema kuwa wanachama wa CCM na CHADEMA ni Watanzania na ndugu. Alidai kuwa hata Mwenyekiti wa CHADEMA ana mtoto aliyezaa na mtoto wa mmoja wa viongozi wakubwa wa CCM, jambo analosema linaonyesha kuwa uadui wa kisiasa unaojengwa kwa wananchi ni wa kutengenezwa.
Alisisitiza kuwa wakati wananchi wanachochewa kugombana, viongozi wao wanaendelea kuishi kwa amani, furaha na ustawi.
Katika hitimisho lake, Mchange alifichua kuwa wenyeviti wa CHADEMA wa ngazi ya mikoa tayari wamefanya mkutano kwa njia ya mtandao na kuazimia kutokukubali kuendelea kutumika na viongozi wa juu wanaodaiwa kulazimishwa kufuata matakwa ya Heche.
Badala yake, amesema wako tayari kujitokeza hadharani kukemea masuala yote wanayoona hayaleti mshikamano wala maslahi mapana ya chama chao.



0 Comments