Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo, ameagiza miradi mbalimbali ya kilimo, ikiwemo miradi ya umwagiliaji, kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ili kuleta ukombozi wa kweli kwa wakulima nchini kiuchumi.
Waziri Chongolo amesema hayo, Desemba 10, 2025, jijini Dodoma wakati wa kikao kazi na viongozi kutoka Ofisi ya Mageuzi ya Kilimo (ATO), Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo (ADF), pamoja na Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF).
Ameielekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) kuhakikisha kuwa miradi yote ya umwagiliaji inayotekelezwa inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaostahili ili iweze kuleta matokeo chanya kwa wakulima na kwa Taifa kwa ujumla. Aidha, amesisitiza umuhimu wa NIRC kufanya ufuatiliaji wa karibu wa miradi yote ili kubaini kwa uhakika manufaa yanayotokana na uwekezaji wa Serikali.
Vilevile, ameiagiza NIRC kuanza mchakato wa kutambua mito yote nchini inayoweza kutumika katika kukuza na kuendeleza uzalishaji wa mazao kupitia umwagiliaji, hatua ambayo itachochea ukuaji wa Sekta ya Kilimo.
Kwa upande wa Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF), Waziri Chongolo ameutaka mfuko huo kuendelea kutoa mikopo yenye tija kwa wakulima na kuimarisha ufuatiliaji wa mikopo hiyo ili kuhakikisha inarejeshwa kwa wakati, kwa kuwa urejeshaji mzuri utaiwezesha Serikali kuongeza mtaji wa mfuko huo kwa lengo la kuwafikia wakulima wengi zaidi.
0 Comments