Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla amemshukuru Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mapinduzi makubwa kwenye sekta ya afya Mkoani Arusha, huku Hospitali ya Wilaya ya Meru Wilayani Arumeru ikipokea shilingi Milioni 900 zilizotolewa kuboresha miundombinu ya huduma za afya hospitalini hapo.
CPA. Makalla ameyaeleza hayo leo Jumanne Septemba 09, 2025 alipotembelea na kukagua hali ya utoaji na uoatikanaji wa huduma kwenye majengo mapya manne ya Hospitali hiyo ikiwemo Jengo la wagonjwa wa nje, Jengo la Maabara, Jengo la Bohari ya dawa pamoja na jengo la kuchomea taka pamoja na jengo la wagonjwa wa dharura, majengo ambayo tayari yameanza kutoa huduma kwa wagonjwa, yakitajwa kupunguza muda wa utoaji wa huduma kwa mgonjwa kutoa saa nane hadi saa mbili.
"Faida za uwekezaji huu mkubwa ni pamoja na kupunguza masaa ya kuwahudumia wagonjwa kutoka saa nane mpaka saa mbili, uwepo wa vipimo 38 ambavyo vimepunguza rufaa za wagonjwa kwenda kwenye hospitali za rufaa kama vile KCMC na Mount Meru, haya ni mafanikio makubwa kwa serikali yetu, niwaombe watoa huduma wote kupitia uwekezaji na maboresho haya, vitafsiriwe kwa ninyi kutoa huduma bora kwa wagonjwa, kuanzia mapokezi, lugha nzuri mpaka kwenye huduma za matibabu." Amesema CPA. Makalla.
Aidha, CPA Makalla, amesisitiza kuwa, mapinduzi hayo makubwa kwenye sekta ya afya yameambatana na ongezeko kubwa la bajeti kwaajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba katika hospitali hiyo pamoja na ukarabati wa jengo la watoto njiti na watoto wachanga wenye kuhitaji uangalizi maalumu.
Awali akisoma taarifa ya Hospitali hiyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Elisante Fabian licha ya kumuahidi Mkuu wa Mkoa utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa wa Meru na maeneo ya jirani, ameeleza faida za maboresho hayo kuwa ni pamoja na kuongeza wigo wa utoaji wa huduma na idadi ya wagonjwa, ongezeko la mapato ya Hospitali, kupunguza muda wa kuhudumia mgonjwa kutoka saa nane hadi saa mbili pamoja na kuiwezesha hospitali hiyo kumudu kufanya vipimo vyote 38 vinavyohitajika katika Hospitali za Wilaya nchini.

.jpeg)

.jpeg)
0 Comments