Zaidi ya watu 10 wamefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya moto mkubwa kuzuka wakati wa sherehe ya harusi katika Manispaa ya Lingwala, jijini Kinshasa, usiku wa kuamkia Jumamosi.
Mkuu wa Manispaa ya Lingwala, Norbert Nzindula, amesema idadi kamili ya watu waliofariki na kujeruhiwa bado haijathibitishwa rasmi, huku mamlaka zikiendelea kufanya tathmini kufuatia ajali hiyo.
Mashuhuda wa tukio hilo wamesema hali ya taharuki ilitawala ndani ya jengo hilo la ghorofa mbili baada ya moto kuanza kusambaa kwa kasi, huku moshi mzito na miali ya moto ikiwaweka wageni katika mazingira magumu ya kujiokoa.
Baadhi ya waliohudhuria walilazimika kukimbia kwa haraka kutoka ndani ya jengo hilo, huku juhudi za uokoaji zikifanyika katika mazingira ya hatari.
Moto huo umeacha sehemu kubwa ya jengo ikiwa imeharibika vibaya, na kuongeza hofu kuhusu usalama wa majengo na mifumo ya umeme katika mji wa Kinshasa.
Kinshasa imekuwa ikishuhudia matukio ya moto mara kwa mara, huku changamoto za miundombinu ya umeme, pamoja na miunganisho isiyozingatia viwango vya usalama, zikitajwa miongoni mwa sababu zinazochangia baadhi ya majanga hayo.
Mamlaka zinaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha moto huo pamoja na idadi kamili ya waathirika.
.jpeg)
0 Comments