Hali ya taharuki imeibuka katika kituo cha mafuta kilichopo Kihonda Viwandani, Manispaa ya Morogoro, baada ya dereva wa lori, Feisal Jabir, mwenye umri unaokadiriwa kuwa kati ya miaka 35 na 40, kudaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na mlinzi wa kituo hicho.
Tukio hilo limetokea leo, Septemba 9, 2026, ambapo kwa mujibu wa baadhi ya mashuhuda, akiwemo Bakara Hussein, marehemu alikuwa amepaki lori lake katika kituo hicho kabla ya kuelekea msikitini.
Mashuhuda hao wanadai kuwa baada ya kurejea kutoka msikitini, kulitokea malumbano kati ya marehemu na mlinzi wa kituo hicho. Inadaiwa kuwa wakati wa mvutano huo, mlinzi huyo alifyatua risasi na kumpiga dereva huyo akiwa ndani ya gari.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa dereva huyo alipoteza maisha kutokana na majeraha aliyoyapata.
Kaimu Afisa Habari wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Scolastica Ndunga, amethibitisha kuwa hospitali hiyo imepokea mwili wa marehemu kwa ajili ya taratibu zinazohusiana na tukio hilo.
Kwa mujibu wa Ndunga, mwili huo ulikuwa na jeraha katika eneo la kichwa.
Tukio hilo limezua maswali na taharuki miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, huku ikisubiriwa taarifa rasmi zaidi kutoka kwa mamlaka husika kuhusu chanzo cha malumbano hayo na hatua zitakazochukuliwa dhidi ya anayehusika.
.jpeg)
0 Comments