Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Sabatho Malima Emmanuel, mwenye umri wa miaka 32 na mkazi wa Buswelu, Wilaya ya Ilemela, kwa tuhuma za kuendesha gari huku akitumia simu ya mkononi na kuandika ujumbe wa lugha chafu akiwa barabarani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, Sabatho ni dereva wa basi la Kampuni ya Obadia, lenye namba za usajili T 870 DVW, aina ya Yutong, linalofanya safari kati ya Mwanza na Nyamongo mkoani Mara.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa dereva huyo alionekana akitumia simu ya mkononi wakati akiendesha, kitendo kinachodaiwa kuwa cha hatari na kuhatarisha usalama wa abiria pamoja na watumiaji wengine wa barabara.
Tukio hilo linadaiwa kutokea Septemba 5, 2026, majira ya saa 6:40 mchana, katika eneo la Isangijo, Wilaya ya Magu, kwenye barabara ya Mwanza–Musoma, wakati basi hilo likitokea Nyamongo kuelekea Mwanza.
Baada ya tukio hilo kubainika, dereva huyo alikamatwa katika eneo la Lamadi, mkoani Simiyu, na anaendelea kushikiliwa na Polisi.
Hatua za kisheria zinatarajiwa kuchukuliwa dhidi yake kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Usalama Barabarani.
Jeshi la Polisi limeendelea kusisitiza umuhimu wa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuepuka matumizi ya simu wakati wa kuendesha, kutokana na hatari kubwa inayoweza kusababisha ajali na kupoteza maisha.
.jpg)
0 Comments