ACT Wazalendo imesema kuna viashiri vikubwa vya rushwa katika ujenzi na usimamizi wa barabara za lami nchini na imemtaka Waziri Mkuu kuchukua hatua za haraka na kuagiza uchunguzi wa kina kuhusu kandarasi za barabara, matumizi ya fedha za umma na ubora wa kazi zinazotekelezwa.
Chama hicho kimesema hali ya barabara kujengwa kwa gharama kubwa na kuanza kuharibika ndani ya muda mfupi haiwezi kuendelea kuitwa uzembe wa kawaida, wakati kuna uwezekano wa mianya ya rushwa katika utoaji na usimamizi wa kandarasi.
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, ambaye pia ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ndugu Ado Shaibu Ado, amesema Serikali inapaswa kutoa majibu kwa wananchi kuhusu sababu za barabara nyingi zinazojengwa kwa fedha nyingi za walipa kodi kushindwa kudumu.
Ado amesema Waziri Mkuu anapaswa kuingilia suala hilo na kuhakikisha uchunguzi unafanyika kuanzia kwenye mchakato wa zabuni, thamani ya mikataba, uteuzi wa wakandarasi, usimamizi wa kazi, vyeti vya malipo, ubora wa vifaa na sababu za barabara kuharibika muda mfupi baada ya kukamilika.
Ado ametoa kauli hiyo alipohutubia wananchi wa Dutwa, Jimbo la Bariadi Vijijini, waliojitokeza katika Mkutano wa Hadhara wa ACT Wazalendo Septemba 11, 2026.

0 Comments