RAIS SAMIA AZINDUA RASMI BWAWA LA JNHHP

 

 Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP) kimezinduliwa rasmi leo Jumamosi, tarehe 22 Agosti, 2026, na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika eneo la Rufiji mkoani Pwani.

Hatua hii inadhihirisha mabadiliko makubwa na ya kihistoria katika sekta ya nishati nchini, kupitia mradi huo wa kimkakati wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 kupitia mitambo tisa, ambapo kila mtambo una uwezo wa Megawati 235.

Mradi huo umegharimu takribani Shilingi trilioni 7.452 za fedha za ndani za Serikali ya Tanzania, ambapo ujenzi wake ulianza rasmi Juni 2019 na kukamilika kikamilifu Machi 2025.

Uzinduzi huo unaashiria dhamira ya dhati ya Serikali ya kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuchochea uwekezaji wa viwanda, na kukuza uchumi wa taifa kwa ujumla.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Nishati, hadi kufikia Mei 31, 2026, JNHPP ilikuwa imechangia takriban asilimia 44.9 ya umeme wote unaozalishwa na kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa, hatua iliyosaidia kufikisha jumla ya uwezo wa uzalishaji umeme nchini kuwa megawati 4,646 na kupunguza changamoto za mgao.

Pamoja na kutumia teknolojia ya kisasa katika uendeshaji wake, kituo hicho kimekuwa kielelezo cha utaalamu wa ndani kwani kinaendeshwa na kusimamiwa na Watanzania kwa asilimia 100.

Mbali na kutoa nishati ya umeme, mradi wa JNHPP unatarajiwa kuleta faida mseto kijamii na kiuchumi, ikiwemo kudhibiti mafuriko katika Bonde la Rufiji, kuendeleza kilimo cha umwagiliaji, pamoja na kuchochea fursa mpya za utalii.

Kutokana na ukubwa wake, Kituo cha JNHPP kinashika nafasi ya tano kwa ukubwa barani Afrika, hatua inayoweka jina la Tanzania kwenye ramani ya dunia katika miundombinu mikubwa na endelevu ya nishati.




Post a Comment

0 Comments