Na Moshi saidi,DAR ES SALAAM.
Kampuni ya Roby One Pharmacy imeendelea kuonyesha dhamira yake ya kuinua mchezo wa ndondi nchini baada ya kuwazawadia mabondia Richard Mtangi na Yohana Mchanja"Computer" zawadi mbalimbali za hamasa kufuatia ushindi na kiwango bora walichoonyesha katika maonyesho ya Mafia Boxing.
Mkurugenzi wa Roby One Pharmacy, Robert Patrick Muchunguzi, ndiye aliyekabidhi zawadi hizo ikiwa ni sehemu ya kuwatia moyo mabondia hao kuendelea kufanya vizuri na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika medani za kimataifa.
Richard Mtangi, ambaye kwa sasa anashika nafasi ya 17 duniani katika uzani wake, namba moja Afrika na namba moja Tanzania, alizawadiwa runinga pamoja na king'amuzi cha Azam TV, zawadi alizochagua mwenyewe kwa ajili ya familia yake.
Akizungumza baada ya kupokea zawadi hizo, Mtangi alimshukuru Mwenyezi Mungu pamoja na Roby One Pharmacy kwa kuthamini juhudi za wanamichezo na kueleza kuwa zawadi hizo zitampa hamasa zaidi ya kuendelea kupambana ili kutimiza ndoto ya kuwa bingwa wa dunia.
"Namshukuru Mwenyezi Mungu na pia Roby One Pharmacy kwa kutuonyesha kuwa wanathamini juhudi zetu. Zawadi hizi zinatupa nguvu ya kuendelea kupigana kwa moyo wote.
Familia yangu sasa itaweza kushuhudia mapambano yangu kupitia TV niliyochagua," alisema Mtangi.
Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo, Mkurugenzi wa Roby One Pharmacy, Robert Patrick Muchunguzi, alisema kampuni hiyo itaendelea kusimama bega kwa bega na mabondia wanaofanya vizuri kwa kuwapatia motisha itakayowasaidia kufikia mafanikio makubwa zaidi.
"Mtangi ni fahari ya Tanzania.Ni namba moja Afrika, namba moja Tanzania na yupo miongoni mwa mabondia bora duniani.
Tunataka kumuona akifika kileleni na kuwa bingwa wa dunia. Ndiyo maana Roby One Pharmacy itaendelea kumpa sapoti pamoja na mabondia wengine wanaofanya vizuri," alisema Muchunguzi.
Kwa upande wake, Yohana Mchanja"Computer" alisema zawadi hizo zimeongeza ari yake ya kuendelea kupambana na kuahidi kuendelea kuwapa furaha Watanzania kupitia ushindi wake ulingoni.
Mchanja pia alisimulia mazungumzo aliyofanya na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, baada ya pambano lake la Super Dome.
"Waziri Mkuu alikuwa ananiuliza zile combination nilizokuwa napiga ulingoni zinaitwaje. Nikamwambia ile ilikuwa ni combination ya hatari," alisema Mchanja huku akitabasamu.
Muchunguzi alitoa wito kwa makampuni mengine, wadau wa michezo na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuwaunga mkono wanamichezo, akisema motisha ni moja ya nyenzo muhimu za kuibua mabingwa wa kimataifa na kuendelea kuitangaza Tanzania kupitia mchezo wa ndondi.

0 Comments