Mfanyabiashara na mkazi wa Butimba jijini Mwanza, Elizabeth Chacha Mugusuhi (30), amehukumiwa kifungo cha nje cha miezi sita baada ya Mahakama kumtia hatiani kwa makosa ya kutoa taarifa za uongo pamoja na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Mahakama ilielezwa kuwa Julai 25, 2026, Elizabeth alifika katika Kituo cha Polisi Nyegezi na kutoa taarifa za uongo akidai kuwa alikuwa ametekwa. Aidha, alidaiwa kutumia taarifa hiyo kuwaomba watu wamtumie kiasi cha shilingi 800,000, akinuia kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Baada ya kusomewa mashitaka yanayomkabili, mshtakiwa alikiri makosa yote mbele ya mahakama. Katika ombi lake la kupunguziwa adhabu, alieleza kuwa hilo ni kosa lake la kwanza na kwamba ana watoto wanaomtegemea, hivyo kuiomba mahakama imuonee huruma.
Akitoa hukumu, Hakimu Mfawidhi John Mgonya alimhukumu Elizabeth kutumikia kifungo cha nje cha miezi sita sambamba na kufanya kazi za huduma kwa jamii kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa na mahakama.
Hakimu huyo alionya kuwa endapo mshtakiwa atashindwa kuzingatia masharti ya kifungo cha nje au atakiuka masharti yoyote ya adhabu hiyo, atalazimika kutumikia kifungo cha ndani gerezani kwa mujibu wa sheria.

0 Comments