Na Ally Mandai.
Meneja wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, ameendelea kuongeza hamasa kuelekea tamasha la Simba Day baada ya kutangaza kuwa ataingia uwanjani kwa mtindo wa kipekee utakaovuta hisia za mashabiki.
Ahmed Ally amesema kuwa katika siku hiyo maalumu, ataingia ndani ya uwanja akiwa amebebwa kwa usafiri wa ungo, akieleza kuwa ni sehemu ya burudani na maandalizi ya kuwapa mashabiki wa Simba tukio la kukumbukwa.
Kauli hiyo tayari imezua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wa soka na watumiaji wa mitandao ya kijamii, ambapo baadhi wameipokea kama sehemu ya ubunifu na kuongeza ladha ya tamasha hilo, huku wengine wakisubiri kuona namna ahadi hiyo itakavyotekelezwa siku ya tukio.
Simba Day ni moja ya tukio kubwa La kila mwaka kwa Klabu ya Simba, yakihusisha utambulisho wa kikosi kipya, burudani mbalimbali pamoja na michezo ya kirafiki inayowakutanisha mashabiki kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania na nje ya nchi.
Kwa kauli yake hiyo, Ahmed Ally ameongeza hamasa kuelekea tamasha hilo, huku mashabiki wakisubiri kwa shauku kuona iwapo kweli ataingia uwanjani kwa usafiri wa ungo kama alivyoahidi. Tukio hilo linatarajiwa kuwa miongoni mwa vivutio vitakavyozungumziwa zaidi wakati wa Simba Day.

0 Comments