Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewapongeza walimu, wanafunzi, wazazi na wadau wa elimu kwa kuuwezesha mkoa huo kutwaa ubingwa wa mashindano ya UMISETA mara tano mfululizo, akisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano na uwekezaji katika elimu na michezo.
Mhe. Mtanda ametoa pongezi hizo wakati akiwapokea walimu 48 kutoka Zanzibar waliowasili mkoani Mwanza kwa ziara ya mafunzo yenye lengo la kujifunza mbinu zinazochangia mafanikio ya Mkoa wa Mwanza katika sekta ya elimu pamoja na kutembelea vivutio vya utalii.
Akizungumzia matokeo ya Kidato cha Sita mwaka huu, amesema Mkoa wa Mwanza ulikuwa na watahiniwa 6,422, ambapo wanafunzi 3,667 sawa na asilimia 57 walipata Daraja la Kwanza, 2,163 Daraja la Pili na 568 Daraja la Tatu.
Ameeleza kuwa ufaulu wa Daraja la Kwanza hadi la Tatu umefikia asilimia 99.9, hali inayoendelea kuifanya Mwanza kuwa miongoni mwa mikoa vinara katika matokeo ya mitihani ya Kidato cha Nne na Kidato cha Sita nchini.
Aidha, amezipongeza Shule za Sekondari Nsumba, Sengerema na Ngaza kwa kuongoza kwa ufaulu, huku wanafunzi 148 wakipata Daraja la Kwanza lenye pointi kati ya 3 na 5.
Mhe. Mtanda amesema mafanikio ya Mwanza hayaishii kwenye elimu pekee, bali pia katika michezo na utamaduni, ambapo mkoa umeendelea kutwaa ubingwa wa UMISETA mara tano mfululizo.
Ameongeza kuwa kikundi cha ngoma cha Kanindo kutoka Wilaya ya Nyamagana kimeendelea kufanya vizuri kwa kutwaa ubingwa kwa miaka mitano mfululizo, jambo linalodhihirisha namna Mwanza inavyoenzi na kuhifadhi utamaduni wa Mtanzania.

0 Comments